Maria Fransiska wa Madonda Matano

Sanamu ya Maria Fransiska wa Madonda Matano.

Maria Fransiska wa Madonda Matano (aliishi Napoli, Italia, tangu azaliwe tarehe 25 Machi 1715 hadi kufa tarehe 6 Oktoba 1791) alikuwa mwanamke ambaye watu wa Napoli walimheshimu hasa kutokana na maisha yake ya sala na upendo wake kwa Mungu na kwa maskini wa mitaa ya matabaka ya chini.

Aligusa watu pia kwa uvumilivu wake mkubwa mbele ya maumivu na mapingamizi mengi na ya mfululizo na kwa malipizi aliyoyafanya kwa wokovu wa wengine[1].

Kutokana na sifa zake, kisha kukusanya ushahidi wa maadili yake ya kishujaa na wa miujiza iliyozidi kutokea kwa maombezi yake, tarehe 12 Novemba 1843 alitangazwa na Papa Gregori XVI kuwa mwenye heri na tarehe 29 Juni 1867 alitangazwa na Papa Pius IX kuwa mtakatifu bikira.

Sikukuu yake huadhimishwa kila mwaka tarehe 6 Oktoba[2].

Anaombwa hasa na wanawake tasa wanaotamani kupata mtoto.

  1. https://www.santiebeati.it/dettaglio/90242
  2. Martyrologium Romanum

From Wikipedia, the free encyclopedia · View on Wikipedia

Developed by Tubidy